TAFAKARI YA SIKU JUMANNE YA JUMA LA 6 LA MWAKA 18/02/2019

Wapendwa Taifa la Mungu karibuni katika tafakari ya masomo yetu ya leo,siku ya jumanne ya juma la 6 la mwaka-tarehe 19/02/2019. Somo la kwanza ni la kitabu cha Mwanzo 6:5-8, 7:1-5, 10 na somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mtakatifu Marko 8:14-21. Tusikilize Injili...

 

Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, saba. Akawaambia, hamjafahamu bado?

Neno la Bwana…   Sifa kwako Ee Kristo.   

  

Wapendwa taifa la Mungu, tafakari yetu ikijikita kwa namna ya pekee katika somo la Injili tulilosikia, tunapata mafundisho makuu mawili, yaani kwanza ushawishi wetu na wenzetu katika jamii na pili namna yetu katika kulisikiliza na kulisoma neno la Mungu.

 

Tukianza na wazo la kwanza yaani ushawishi wetu na wenzetu katika jamii, mitume wanataadharishwa na Bwana wetu Yesu Kristo juu ya chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Neno chachu katika Biblia Takatifu limetumiwa na Bwana wetu Yesu Kristo katika mafundisho na mifano yake likiwa na maana mbili tofauti, yaani chachu iliyo njema (Mt.13:33 na Lk. 13:20) na chachu isiyo njema (Mk 8:15).

 

Kristo anatumia neno CHACHU akimaanisha ushawishi waliokuwa nao Mafarisayo na Herode katika jamii, hasa kwa kumuuliza maswali ya kumtega kila mara na hasa likiwemo lilile la kuhitaji ishara kutoka juu. Jambo la kizazi kinacho hitaji ishara kutoka juu, tunapata simulizi lake kutoka Injili ya Mtakatifu Marko 8:11-13, linamuumiza na kumpelekea atoe taaadhari kwa wafuasi wake juu ya ushawishi au chachu hiyo isiyo njema na hatarishi baina yao.

 

Tujiulize mimi na wewe katika jamii zetu tunatumiaje vipaji na uwezo aliotuzawadia Mwenyezi Mungu katika jamii? Pengine tunavitumia vipaji vyetu kuleta mgawanyiko na mafarakano katika jamii zetu na hivo kuhatarisha amani katika jamii zetu tunamoishi, maana Mafarisayo na Herode walitumia akili kama zawadi toka kwa Mungu kutunga maswali na kuandaa mitego mbalimbali ya kuweza kumkamata Bwana wetu Yesu Kristo.

 

Na pia tuutilie maanani ushauri wake Yesu Kristo juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya chachu isiyo njema. Katika kuuitikia mwaliko huu, tujilinde na ushawishi wa utandawazi na kila kitu chenye mwelekeo wa kupoteza zawadi za imani na amani tulizozawadiwa na Mwenyezi Mungu katika jamii zetu. Hili litafanikiwa hasa kwa kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kutufunulia katika jamii zetu vitu na watu, wenye malengo ya kutupeleka katika hali ya kuzipoteza zawadi za amani na imani katika jamii zetu, ili daima tudumu katika kuchukua tahadhari dhidi yao. 

 

Wapendwa taifa la Mungu, haikuwa rahisi kwa wafuasi wa Bwana wetu Yesu Kristo kuelewa kile alichomaanisha wakati akiwatahadharisha juu ya chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Hawakuweza kuelewa kwani mawazo yao waliyakita zaidi katika kuyafikiria mambo ya kidunia yaani mikate na hivo kushindwa kuelewa ujumbe waliokuwa wakiambiwa. Wao kama wafuasi wa Yesu Kristo walitakiwa kuwa na imani thabiti kwamba Yesu angewalisha pamoja na kwamba hawakuwa na mikate chomboni. Ndio maana Yesu anachukua jukumu la kuwakumbusha matukio aliyokwisha yafanya kwa kuwalisha ili yakomaze imani yao katika uweza wake.

 

Wapendwa taifa la Mungu, Tujiulize mimi na wewe ni mambo mangapi yanatutawala katika maisha yetu hadi tunashindwa kutenga muda wa kulitafakari na kulisoma neno la Mungu? Mambo hayo yaweza kuwa ni ndugu, jirani, marafiki, chakula, kazi na vitu vyote vya ulimwengu huu kwa ujumla. Baada ya kuyatambua mambo hayo ndipo tukumbuke kuchukua tahadhari dhidi ya chachu yake kama mwaliko wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa wafuasi wake.

 

Hivyo basi ni mwaliko kwetu sisi sote leo na daima kudumu katika kumtumainia na kumuomba Bwana wetu Yesu Kristo, atufunulie wale maadui wa imani na amani. Na atujalie nguvu tupate kuvirithisha vizazi vijavyo imani hii, kama mitume walivyofanya kwetu sisi. Na daima tutenge muda wa kulisoma na kulitafakari neno la Mungu, kwani ndilo taa na msingi wa imani yetu Wakristo.

Tumsifu Yesu Kristo…  

   

 Tafakari hii imetolewa nami: Frt Enock Mutegeki Richard

      Jimbo Kuu la Mwanza

     mwaka wa pili Teolojia

     Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora.  

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.