TAFAKARI YA SIKU IJUMAA YA JUMA LA 4 LA MWAKA 08/02/2019

WAPENDWA TAIFA LA MUNGU Tumsifu Yesu Kristo karibuni katia TAFAKARI YA NENO LA MUNGU ijumaa ya juma la nne mwaka c wa kanisa somo la  injili ya Mk. 6:14-29.   Ijumaa 08.02.2019

WAZO KUU KATIKA INJILI YA LEO NI TUSIMAMIE UKWELI

Katika Injili ya leo tunapata simulizi ya kuuawa kwa Yohane Mbatizaji. Simulizi inayofuata mara baada ya wale Thenashara kutumwa. Hii ni kutaadharisha kuhusu gharama za ufuasi. Kujitoa sadaka hata kutoa uhai kwasababu ya ukweli wa injili. Simulizi la kuuawa kwa Yohane Mbatizaji ni fundisho kwa kila mbatizwa kutetea ukweli wa injili  hata kutoa uhai kwa ajili ya kusimamia ukweli.

Yohane Mbatizaji anauawa kwa sababu ya kusimamia ukweli. Anaufahamu ukweli, anausema na kuusimamia bila kujali cheo, hadhi, au jina la mtu. Anamkemea Herode kwamba si halali kuwa na mke wa nduguye yaani Herodia. Ukweli huu unamfadhaisha Herodia na hatimae anatafuta kumuua Yohane Mbatizaji.

Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Herode (birthday) anafanya karamu na anawaalika majemedari na wenye vyeo wa Galilaya. Binti Herodia anacheza vizuri anawavutia wageni waliokuwepo. Mfalme kwa viapo anamuahidi kumpatia atakacho hata kama ni nusu ya ufalme wake. Binti huyu anamuuliza mamaye aombe nini, mamaye anamjibu kichwa cha Yohane Mbatizaji. Kwa sababu ya viapo alivyokuwa amevifanya inamlazimu aagize Yohane Mbatizaji akatwe kichwa, na inafanyika hivyo. Kinacho sikitisha hapa ni Herode kuona viapo vyake kuwa muhimu kuliko uhai wa Mtu.ukweli unamwangamiza Yohane mbatizaji.

Tunaaswa katika Injili ya leo tuwe jasiri katika kusema ukweli. Tusimamie ukweli bila kuupindisha, kuuonea haya, au kutafuna maneno. Tuusimamie hata kama itatulazimu kutoa sadaka kubwa. Tujifunze kwa Yohane Mbatizaji kusema na kusimamia ukweli bila kujali cheo cha mtu, urafiki, jina   la mtu wala hakujali muda kwa sababu ukweli hauna muda maalum, saa yake ni sasa, ni kila wakati.

Tusiogope kusema ukweli na kuusimamia. tusiogope macho ya watu, vyeo vyao, wala majina yao.  Tusiogope watu watanionaje, watanifikiriaje, au nitakuwa niko kinyume na wenzangu. kuogopa huku  huleta madhara makubwa katika jamii na hata husababisha kifo. Yohane Mbatizaji hakumwogopa Mfalme, anampa ukweli wote.

Tukumbuke kwamba hata kama tutaogopa kusema ukweli, tukauficha, Ukweli hujisimamia wenyewe. Ukweli haufi; ukweli utapanda na kuelea juu ya uongo kama mafuta yanavyo kuwa juu ya maji. Hata kama tutauzika ukweli kaburini, hauta kaa huko. Yohane Mbatizaji anatufundihsa tusimamie ukweli hata inapotudai sadaka kubwa. Heshima tunayoweza kuupa ukweli ni kuusema na kuusimamia; tusiogope kukosoa na kukemea maovu katika jamii kwa haki na ukweli. Hii itatusaidia kujenga jamii inayojitambua zaidi.

Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Katika jamii yetu ya leo mambo ni tofauti; mkweli anaonekana kama adui anaepaswa kushughulikiwa au kuwindwa na kuangamizwa kwa namna yoyote ile. Lazima kufahamu kwamba ukweli ni tawi la maadili na niwa muhimu sana katika jamii. Tunatakiwa  tuwe wa kweli kwanza kwetu sisi wenyewe ndipo tuseme ukweli juu ya wengine. Tujifunze kupokea ukweli bila chuki wala manungÔÇÖuniko na tuwe tayari kubadiliaka. Tumwombe Mungu kwa maombezi ya Mt.Yohane Mbatizaji atujalie tuwe wa kweli katika yote tufanyayo. Tuseme na tuutetee ukweli daima, kwani ukweli utatuweka huru. Yohana 8:32

Tafakari hii imeletwa kwenu nami FRT. DEOGRATIAS MIKU wa JIMBO KATOLIKI MOSHI, MWAKA WA II WA THEOLOJIA SEMINARI KUU KIPALAPALA.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.